HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. DKT. JAKAYA
MRISHO KIKWETE WAKATI WA UZINDUZI WA CHAPISHO LA TATU LA TAARIFA ZA MSINGI ZA
KIDEMOGRAFIA, KIJAMII NA KIUCHUMI LINALOTOKANA NA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA
MWAKA 2012, TAREHE 10 JUNI, 2014
Chanzo :Ikulu
Mheshimiwa Waziri Mkuu;
Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar;
Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi;
Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mawaziri Waliopo;
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;
Waheshimiwa Mabalozi;
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi;
Katibu Mkuu Kiongozi na Makatibu Wakuu;
Viongozi wa Serikali wa Ngazi Mbalimbali;
Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi;
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu;
Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Viongozi wa Madhehebu ya Dini;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
SHUKRANI NA PONGEZI
Ndugu Wananchi;
Awali ya yote, naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi
Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa siku ya
leo. Napenda pia kuwashukuru waandaaji wa hafla hii kwa kunipa heshima
kubwa ya kuzindua Chapisho la Tatu la Taarifa za Msingi za Kidemografia,
Kijamii na Kiuchumi Linalotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.
Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maelezo
yako mazuri ya awali kuhusu Chapisho hili. Nakupongeza wewe, pamoja na Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa uongozi wenu mzuri wa zoezi la Sensa. Chapisho
tunalozindua leo ni matunda ya kazi nzuri mliyoifanya ya kuziongoza Idara za
Takwimu za Serikali zetu mbili ambazo ndizo zilizosimamia na kuendesha zoezi
lenyewe la sense ya watu na makazi.
Sensa inaendeshwa kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha
Sheria ya Takwimu (the Statistic Act) sura ya 351. Katika kipindi
chote cha miaka 50 ya Muungano wetu tumefanya Sensa mara tano, mwaka 1967,
1978, 1988, 2002 na 2012.
Umuhimu wa Chapisho la Tatu
Ndugu Wananchi;
Sensa ni zoezi pana sana. Sensa ni zaidi ya
kuhesabu watu. Sensa hujumuisha pia kukusanya na kufanya uchambuzi wa
taarifa kuhusu masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii. Taarifa hizo
husaidia Serikali katika utungaji wa sera na kutengeneza mipango na mikakati ya
maendeleo nchini. Tangu kufanyika kwa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka
2012, Idara Kuu ya Takwimu ya Taifa na Idara ya Takwimu Zanzibar ambazo ndizo
zilizohusika na zoezi hili zimeendelea kutoa matokeo kulingana na kalenda ya
utoaji wa matokeo ya Sensa. Matokeo ya mwanzo nilitolewa tarehe 31 Desemba,
mwaka 2012 kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja. Siku ile nilitangaza jumla ya idadi
ya watu nchini Tanzania. Chapisho la pili lilihusu mgawanyo wa watu kwa umri na
jinsi ambalo lilitolewa tarehe 25 Septemba, 2013.
Chapisho la Tatu ninalolizindua leo linatoa
taarifa za msingi za kidemografia (mnyumbuliko wa idadi ya watu), kijamii na
kiuchumi zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Taarifa za
Chapisho la Tatu zina umuhimu wa aina yake. Zinaonesha Tanzania imepiga
hatua kiasi gani katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Aidha,
upatikanaji wa taarifa katika kipindi hiki utaviwezesha vizazi vijavyo
kuifahamu Tanzania ilivyokuwa mwaka 2012.
Muhtasari wa Matokeo ya Chapisho la Tatu
Ndugu Wananchi;
Sensa ya Mwaka 2012 imefanyika katikati ya utekelezaji
wa Mpango wa Taifa wa Miaka 5 (2011-2016). Mpango huu tunaoendelea kuutekeleza
una lengo la kutufikisha kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na ile
ya Zanzibar ya mwaka 2020 ambapo tunatarajia kuwa nchi yetu itakuwa imefikia
uchumi wa kati. Kwa utaratibu huu wa kufanya Sensa kila baada ya miaka 10, ina
maana kuwa Sensa inayofuata itafanyika mwaka 2022 ikiwa ni miaka michache kabla
ya kufikia Dira ya Taifa. Hivyo, matokeo haya ni msingi wa kupima mwelekeo wetu
kiuchumi na kijamii kufikia lengo letu la kuwa uchumi wa kati ifikapo 2020 kwa
upande wa Zanzibar na 2025 nchi nzima.
Chapisho hili lina takwimu nyingi sana kuhusu nyanja
mbalimbali za maisha ya Watanzania. Takwimu hizi zinatupa fursa ya kujua maeneo
tunayofanya vizuri na yale tunayohitajika kuyaimarisha. Vilevile, zinatuonyesha
yale maeneo ambayo tulidhani tunafanya vizuri lakini kumbe siyo, hivyo basi
tunatakiwa kuyawekea mkakati maalum. Hali kadhalika, taarifa zinatuamsha kuona
yale maeneo mapya ambayo hatukuwahi kuyafikiria lakini sasa tunapaswa
kuyaangalia kwa karibu.
Kwa ujumla, kulingana na takwimu za Sensa ya 2012,
idadi ya watu Tanzania iliongezeka kutoka watu milioni 34.4 mwaka
2002 hadi watumilioni 44.9 mwaka 2012. Hii ni sawa na kasi ya ongezeko la asilimia
2.7 kwa mwaka. Kwa kasi hii ya ongezeko la watu, Tanzania Bara inatarajiwa
kuwa na watu milioni 63.3 mwaka 2025 ambao ndiyo mwaka wa
mwisho wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025 kwa Tanzania Bara. Aidha,
Zanzibar inatarajiwa kuwa na watu milioni 1.8 ifikapo mwaka 2020
ambao ndiyo mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar.
Kwa kasi hii ya ongezeko la idadi ya watu Tanzania inatarajiwa kuwa na watu milioni
125 mwaka 2050.
Ndugu Wananchi;
Ili kufikia dira zetu za maendeleo, yaani ya mwaka 2020
kwa Zanzibar na ya mwaka 2025 kwa nchi nzima ambapo tutakuwa na idadi ya watu
takribani milioni 65.1, inatupasa kujitazama tulipotoka na tulipo leo. Kwa
mujibu wa Chapisho hili la Tatu, tumepiga hatua kubwa na nzuri katika maeneo
mengi, na hivyo kuashiria kuwa tuko katika mstari sahihi kuelekea Tanzania
tunayoitamani. Baadhi ya takwimu hizi kwa ufupi ni zifuatazo:
i. Zaidi ya asilimia
90 ya watu wote Tanzania walizaliwa baada ya Muungano wa mwaka 1964.
Tafsiri yake ni kwamba idadi kubwa ya Watanzania ni vijana ambao wamezaliwa,
kukua na kufaidika na matunda ya Muungano. Hiki ni kiashiria
kikubwa kuwa tumeweza kujenga utaifa mpya, yaani utanzania katika miaka 50 ya
Muungano wetu.
ii. Hii ni
Sensa ya tano tangu Muungano wetu mwaka 1964. Sensa ya kwanza ilikuwa
mwaka 1967, ya pili mwaka 1978, ya tatu mwaka 1988, ya nne mwaka 2002 na ya
tano 2012. Takwimu za Sensa za kati ya mwaka 1967 na mwaka 2012
zinaonesha kuwa idadi ya watu wa Tanzania ambao wanaishi mijini imeongezeka
kutoka asilimia 6 mwaka 1967 hadi asilimia 30 mwaka
2012. Ukuaji huu wa miji ni kiashiria muhimu kuwa safari yetu ya kuelekea
uchumi wa katini ya uhakika. Hatuna budi sasa, sera na mikakati yetu
kuielekeza katika kuhakikisha miji yetu inao uwezo wa kuhimili ongezeko hili la
watu kwa maana ya utoaji wa huduma za kijamii na ajira.
iii. Katika
kipindi cha miaka 50 wastani wa umri wa kuishi kwa mtoto wa Kitanzania
anayezaliwa umeongezeka kutoka miaka 41 mwaka 1967 hadi kufikia miaka 61 mwaka
2012. Maana yake ni kuwa, huduma za afya zimeimarika, watu sasa
wanaishi kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Hata hivyo, bado
hatujafikia viwango vya wenzetu wa Asia na Ulaya ambao wastani wao ni miaka 70
na kuendelea.
iv.
Vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 115 kati
ya kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai mwaka 1988 hadi kufikia vifo45 mwaka
2012. Na, mwaka 2013 tumefikia 21. Vifo vya watoto chini ya miaka 5
vimepungua kutoka 231 mwaka 1988 hadi 68 mwaka 2012 na 2013
tumefikia vifo 54 kwa 1,000. Pia, idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi
imepungua kutoka vifo 578 kwa kila akina mama 100,000 wanaojifungua
mwaka 2004/2005 hadi 454mwaka 2010 na kwa mujibu wa takwimu za
Sensa, vifo hivi vimeendelea kupungua hadi 432 mwaka 2012. Hii ni hatua
kubwa kuelekea lengo la Milenia ya Mwaka 2015 ya vifo 193.
v. Asilimia
ya kaya zinazopata maji safi ya kunywa imefikia asilimia 57 mwaka
2012. Vile vile, kaya zinazotumia umeme kama nishati ya kuangazia
zimeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2002 hadi asilimia
21 mwaka 2012.
vi. Kwa
upande wa sekta ya elimu, asilimia ya watu wenye umri wa miaka 10 na zaidi
wanaojua kusoma na kuandika kwa Tanzania Bara imeongezeka kutoka asilimia
31 mwaka 1967 hadi kufikia asilimia 78 mwaka 2012. Kwa Zanzibar
kiwango hiki kimeongezeka kutoka asilimia 39 mwaka 1967 hadi asilimia
86 mwaka 2012.
vii. Takwimu
zinazoonesha kwamba umaskini wa kipato umepungua kutoka asilimia 33.6 mwaka
2007 hadi asilimia 28.2 mwaka 2012.
viii. Takwimu
zinaonesha kwamba makazi ya wananchi wote wa Tanzania yaliyojengwa kwa vifaa
vya kisasa (zege, mawe, saruji na vyuma) yameongezeka. Familia zinazoishi
kwenye nyumba za bati zimeongezeka kutoka asilimia 46 mwaka 2002 hadi asilimia
65 mwaka 2012.
ix. Vilevile,
umiliki wa simu za kiganjani umeongezeka sana. Mwaka 2012 wastani ulikuwa
ni asilimia 64 ikilinganishwa na asilimia 10mwaka 2005.
Kuongezeka kwa simu ni kiashiria cha kuongezeka kwa biashara, idadi ya watu
wanaotumia huduma za kifedha kwa njia ya simu na urahisi wa mawasiliano ambao
unawezesha usambazaji wa taarifa za kijamii na kibiashara katika maeneo mengi
hivi sasa.
Mazingatio Yatokanayo na Chapisho la Tatu la Sensa
Ndugu Wananchi;
Ufupi au urefu wa safari unaweza kuujua tu iwapo
unafahamu unapotoka, ulipo na unapokwenda. Taarifa ambazo zimewasilishwa
na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kuwa tumepata mafanikio ya kuridhisha
katika maeneo mengi, na kuwa tumekuwa tunasonga mbele mwaka hadi mwaka na siyo
kurudi nyuma. Kwa hiyo matokeo haya yanapaswa kuwaongoza Viongozi
na Watendaji wa ngazi zote katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kujua
maeneo ambayo kasi ya utekelezaji wa programu za maendeleo kwa wananchi ilikuwa
ndogo, na hivyo kustahili kupewa msukumo mpya katika utekelezaji wake.
Ndugu Wananchi;
Nimefarijika kusikia kuwa taarifa za Sensa zinaonesha
hatua kubwa tuliyopiga katika kuleta usawa wa kijinsia kati ya wanaume na
wanawake. Ingawa viashiria vingi bado vinaonekana bora zaidi kwa wanaume kuliko
wanawake, lakini pengo kati yao limepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma. Kwa
mfano, asilimia ya wanaume wenye umri wa miaka 10 na zaidi wanaojua kusoma na
kuandika ilikuwa asilimia 45 kwa Tanzania Bara na asilimia 55 kwa
Zanzibar mwaka 1967. Kwa upande wa wanawake ilikuwa asilimia 19 na asilimia 23 kwa
Tanzania Bara na Zanzibar mwaka 1967. Taarifa za Sensa ya Mwaka 2012 zinaonesha
kuwa pengo hili limepungua sana. Wanaume wenye umri wa miaka 10 na zaidi
wanaojua kusoma na kuandika kwa mwaka 2012 ni asilimia 82 ya wanaume
wote kwa Bara ukilinganisha na asilimia 75 kwa wanawake. Kwa upande
wa Zanzibar, idadi ya wanaume wanaojua kusoma na kuandika ni asilimia 89 ya
wanaume wote kulinganisha naasilimia 83 ya wanawake.
Hatuwezi kupata maendeleo makubwa na endelevu bila
kuhakikisha usawa wa kijinsia. Wanawake ni asilimia 51 ya Watanzania
wote, hivyo, hatuna namna yoyote tunayoweza kulipuuza kundi hili kubwa, ambalo
ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote katika shughuli za maendeleo.
Ndiyo maana, tumeelekeza juhudi kubwa kurekebisha kasoro hii ya kihistoria na
kimfumo kwa kuwapa wanawake fursa ili nao washiriki sawia katika shughuli za
maendeleo katika ngazi ya familia, jamii na hata taifa. Ni vyema
ikaeleweka kuwa hatuwapendelei wanawake bali tunawapatia kile wanachostahili
kupata kama raia na kama wanadamu. Stahili ambazo wamekuwa wakizikosa kwa
miaka mingi.
Serikali itaendelea kuimarisha juhudi za utekelezaji wa
Sera ambazo zinalenga kuhakikisha kuwa pengo hili linazibika ili Watanzania
wote wafaidike na rasilimali za Taifa bila ya kujali jinsia zao.
Maelekezo kwa Tume ya Taifa ya Takwimu
Ndugu Wananchi;
Nimesema hapo awali kuwa lengo kubwa la kufanya Sensa
ni kutoa takwimu ambazo zitachangia katika jitihada za kuboresha maisha ya
Watanzania. Taarifa za sensa ambazo zitasaidia kuboresha sera za nchi kwa
mambo mbalimbali, kupanga na kutathmini programu za maendeleo na uimarishaji wa
utoaji wa huduma za jamii. Lengo hili haliwezi kufikiwa ikiwa taarifa za
sensa na nyinginezo kwa ujumla wake hazitawafikia watumiaji wote wanaozihitaji.
Ofisi za Takwimu zina jukumu la kutoa takwimu katika mfumo mzuri na lugha rahisi
na kuzisambaza na kuhamasisha matumizi yake.
Pamoja na usambazaji wa taarifa za sensa kwa
vitabu na machapisho, tumieni tovuti na njia nyingine za kisasa kusambaza
taarifa zenu. Ninafarijika kusikia kwamba tayari mmeanza juhudi hizi, kwani
uzinduzi wa Chapisho hili la tatu utaenda sambamba na uzinduzi wa usambazaji wa
taarifa kwa njia ya mtandao.
Ofisi za Takwimu zimetimiza wajibu wake wa kutoa
takwimu na sasa ni jukumu la Wizara, Idara,Taasisi za Serikali na watumiaji
wengine wote kuzifanyia kazi. Natoa agizo kwa viongozi ngazi zote za utawala
kutafsiri matokeo haya kwa kuoanisha na utekelezaji wa sera na programu za
maendeleo ya kisekta katika maeneo yao. Matokeo haya ya Sensa sasa ndiyo rejea
yetu ya takwimu katika mipango yetu ya utekelezaji. Kile kisingizio cha
kukosekana kwa takwimu mpya sasa kimefikia ukomo. Takwimu ni kitendea
kazi, sasa mnazo na mkazifanyie kazi, siyo kuendeleza semina za kujadili
matatizo na mapungufu. Takwimu zimetuonyesha mafanikio tuliyoyapata na
mapungufu yaliyopo ambayo mkayatatue na siyo kuyajadili.
Wito kwa Wananchi na Wadau
Ndugu Wananchi;
Napenda pia kutoa wito kwa wananchi na wadau wa
maendeleo hasa asasi za kiraia kusoma taarifa hizi na kuzitumia vizuri.
Kumekuwepo na upotoshaji mkubwa sana wenye kubeza mafanikio yaliyopatikana
nchini kutokana na jitihada za Serikali na wananchi kwenye kuleta
maendeleo. Taarifa hii inaweka wazi ukweli ulivyo. Zitumieni.
Kama upotoshaji ulikuwa ni kwa sababu ya kukosekana kwa rejea ya takwimu
sahihi, takwimu ndizo hizo kwa kila mmoja wetu kuziona na kuzitumia.
Asiyefanya hivyo ana lake jambo.
Hitimisho
Ndugu Viongozi Wenzangu;
Ndugu Wananchi;
Niruhusuni nirudie tena kuwashukuru washirika wetu wa
maendeleo waliotusaidia kufanikisha zoezi la Sensa ya watu na makazi. Kwa
namna ya pekee nawashukuru Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Shirika la
Maendeleo la Uingereza (DFID), Taasisi za Umoja wa Mataifa ikiwemo UNFPA, UNDP
na UNICEF. Nawashukuru tena Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo
Pinda na Makamu wa Rais wa Zanzibar, Balozi Ali Seif Idd kwa uongozi wenu mzuri
uliowezesha zoezi zima la sensa kufanikiwa. Pia, nawapongeza viongozi na
watendaji wa Idara zetu mbili za Takwimu kwa kazi kubwa na nzuri
waliyofanya. Umakini na umahiri wao ndiyo uliotufikisha hapa.
Nawashukuru na kuwapongeza viongozi wote wa Serikali wa ngazi zote za utawala
ambao walishiriki kwa ukamilifu katika maandalizi na hatimaye utekelezaji wa
Sensa ya Mwaka 2012. Nitoe pia shukrani kwa viongozi wa vyama vya siasa,
madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya Kiserikali kwa ushiriki wenu hasa
kwenye hatua ya uhamasishaji wa ushiriki wa umma. Nawashukuru wadau wetu wa
maendeleo kwa michango yao muhimu ambayo imesaidia kufanikisha sensa hii.
Shukrani za kipekee ziwaendee Wananchi wote ambao
walijitokeza kuhesabiwa na kujibu maswali ya sensa kwa ufahamu mkubwa. Kukubali
kwao kushiriki ndiko chanzo kilichowezesha kupatikana taarifa tunazozindua leo
na nyingine zitakazofuata. Ni dhahiri kuwa Serikali yetu imetimiza kwa ufanisi
jukumu la kufanya Sensa ya Watu na Makazi nchini. Lengo limetimia la
kujua hali halisi ya rasilimali watu iliyopo Nchini kama zilivyofanya Awamu zote
zilizotangulia.
Ndugu Wananchi;
Baada ya kusema maneno haya ya utangulizi, sasa, kwa
heshima na taadhima kubwa, napenda kutamka kwamba Chapisho la
Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi linalotokana na Sensa
ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 Pamoja na Matumizi ya Tovuti katika
kupata taarifa mbalimbali za Sensa ya Watu na Makazi limezinduliwa rasmi.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza!
No comments :
Post a Comment