BAADHI ya wakazi wa jijini Tanga, wameomba uongozi wa Wilaya ya Tanga
kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kuweka mkakati endelevu, utakaodhibiti
wimbi la vijana wa kike wanaojiuza miili yao nyakati za usiku kwenye baadhi ya
barabara za katikati ya mji na bustani za kupumzikia.
Wamesema hatua hiyo, itasaidia kukomesha vitendo hivyo vinavyoendelezwa
bila woga na kudhibiti kasi ya ongezeko lao, hasa katika barabara ya
Independence na Bustani ya Forodhani nyakati za jioni.
Aisha Zahoro, mkazi wa Chumbageni alisema hali ni mbaya zaidi katika
Bustani ya Forodhani, ambapo wasichana wadogo hasa wale wenye umri wa kusoma
shule za sekondari, wamefikia hatua ya kuvua nguo zao ili kuonesha wazi
maumbile yao kwa baadhi ya wanaume, wanaofika eneo hilo kwa lengo la
kuwachukua.
“Sikuamini macho yangu usiku wa saa 2 hivi, nikiwa hapo bustanini
nimeketi kwenye viti vilivyoko karibu na miembe mikubwa, pembeni walisimama
wasichana kadhaa nikadhani nao wamekuja kupunga upepo au kupata vyakula hapo.
Lakini kumbe sivyo, wenzangu hao walikuwa kazini…nilishangaa kwani walipofika
wanaume wawili, wenzangu walianza kuzungumza nao biashara, ghafla mmoja kati
yao akafunua nguo alizokuwa amevaa, akitamba kwamba ‘nitazame mimi sina kovu
hata moja mwilini,” alisema.
Alisema wasichana hao wanajiuza kwa bei za kati ya Sh 2,000 kwa huduma
ya haraka (chapchap) hapo hapo bustanini, Sh 5,000 kinyume na maumbile na Sh
10,000 ndani ya gari la mteja.
Alidai kwamba vitendo hivyo, sasa vimevuta wasichana wengi wadogo, ambao
walipaswa kuzingatia masomo.
Hassan Sadoki alisema ili kusaidia kudhibiti hali hiyo, ambayo sasa
inaleta sifa mbaya ndani ya Jiji ni vema ufanywe msako endelevu wa kuwakamata
na kuwaadhibu ili iwe mfano kwa wengine, wanaotaka kuendeleza vitendo hivyo,
kwa lengo la kujipatia fedha ya kujikimu kimaisha.
Kwa upande wake, Audax Msofe, mkazi wa Namiani, alisema binafsi anaamini
vijana wanaofanya biashara ya ngono katika mitaa mbalimbali ya jijini humo,
ikiwemo kwenye bustani, wanahitaji kujengwa kwa maadili ya kidini ili wawe na
hofu ya Mungu.
“Naamini msako wa polisi peke yake hautatosha kuwadhibiti, badala yake
viongozi wa dini nao washirikishwe katika suala hili kwa kuendelea kuzungumza
na waumini wao hasa vijana, ambao hivi sasa wanaonekana hawana kabisa hofu ya
Mungu mioyoni mwao na hivyo kuamua kujiingiza kwenye vitendo viovu”, alisema.
Chanzo: Habarileo
No comments :
Post a Comment