Wednesday, July 23, 2014

WANAFUNZI WATOA YA MOYONI

Wanafunzi wakimpapasa ngamia Snake Park Arusha
RIPOTI YA WANAFUNZI KUHUSU ZIARA YA MAFUNZO KATIKA HIFADHI YA ZIWA MANYARA TAREHE 9 – 11/7/2014 SHULE YA WASIOONA IRENTE



Kwanza tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha katika safari ile ya kutembelea HIfadhi ya Ziwa Manyara tuliyoianza tarehe 9/7/2014 hadi 11/7/2014. Tunachoshukuru sana ni kwenda na kurudi salama bila mtu au watu kuugua kwa maradhi au ajali.
Safari yetu ilianza saa 11:30 alfajiri na kufika saa kumi na moja jioni siku hiyo hiyo. Katika safari hiyo tuliona na kusikia mengi ya kuvutia kama vile viwanja vya ndege kama KIA na Kisongo – Arusha, Panone Super Market, kiwanda cha mkonge Mazinde, Hifadhi ya Mkomazi, Chuo cha elimu maalum Patandi, Chuo kikuu cha Makumira, shule ya viziwi Mwanga, Safu za milima Pare, Mlima Meru na mashamba ya maua Arusha.
Mapokezi: Tulipokelewa na wenyeji kwa ukarimu na wenyeji wetu Manyara
Siku ya pili: Tuliingia ndani ya Hifadhi ya Ziwa Manyara kuona wanyama waliomo pamoja na ndege. Wakati tunaanza kutembelea hifadhi hiyo tulipewe historia fupi ya Hifadhi ya Ziwa Manyara.
Historia ya Hifadhi ya Ziwa Manyara.
Hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka 1960 na Mheshimiwa Mbunge Barongo. Kabla ya mwaka 1960 ilikuwa ni eneo la kuwindia wanyama na ndege. Mwaka 1958 uwindaji huo ulikomeshwa na kufanyika kuwa hifadhi katika mwaka 1960. Neno Manyara limetokana na neno la Kimasai liitwalo IMANYARA ambalo kwa Kiswahili ni mti uitwao MNYAA ambapo kwa kisayansi unaitwa EUPHOBIA TURCALI na kwa jina la kawaida linaitwa FINGER TREE.
Sifa ya Hifadhi ya Ziwa Manyara.
Kwanza hifadhi hiyo ina ukubwa wa Km2 648.7. Hifadhi pekee yenye ndege wengi zaidi ya aina 30 wanaopamba hifadhi pamoja na Ziwa Manyara, Makundi ya wanyama zaidi ya saba wanaoishi pamoja, Simba wanaopanda juu ya miti, Maji ya moto yanatoka kwenye miamba na inapendwa kutembelewa na wanafunzi sana kwa miaka ya hivi karibuni.
Vivutio vilivyopo ndani ya Hifadhi ya Ziwa Manyara.
Katika hifadhi hiyo kuna vivutio vya aina nyingi na baadhi ya vivutio ni Maji moto ya chemchemi, miti yenye sumu, maji ya ardhini yanayolisha misitu ndani ya hifadhi ambayo husaidia kijani kuwepo karibu mwaka mzima, samba wanaopanda juu ya miti, Pundamilia, Ngili, nyati, tembo, twiga, ndege, viboko, nyumbu, swala, mbuni fisi, duma, pamoja na Ziwa Manyara nk.
Changamoto tulizopata
Changamoto tulizopata ni pamoja na vumbi katika hifadhi ,usafi tulioukuta hauridhishi na tulipataa pancha wakati wa kurudi.
Mafanikio
Pamoja na changamoto hizo tumejifunza mambo mengi yakiwemo kujua kila tabia ya mnyama tuliemwona ,tulipata historia ya hifadhi hiyo na kutambua chanzo cha ziwa Manyara. Pia tumeona na kugusa vinyago vinavyochondwa Mto wa Mbu. Wakati tunarudi tulipitia Snake Park Arusha ambapo eneo hilo lina nyoka, mamba, ndege, nyani, ngamia na vibanda vya makumbusho
SHUKRANI
Tunawashukuru waliofanikisha safari hiyo,kwa pamoja tunasema Mungu awabariki.
Mwisho kabisa tunatoa maoni yetu kwamba safari za mafunzo zisiwe mwisho bali ziwe endelevu kwani wanafunzi wanajifunza kwa kugusa kunusa na kuona vitu halisi.
     
Ripoti hii imeandaliwa na wanafunzi wa darasa la V – VII wa shule ya wasioona Irente

No comments :

Post a Comment