www.fahamuhaya.blogspot.com
Mhe. Samia ametoa wito huo leo Jumatano Machi 4,2020 wakati akifungua Kongamano la Kuadhimisha na Kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 baada ya Mkutano wa Beijing linalofanyika katika Ukumbi wa Hyatt Regency Hotel Jijini Dar es salaam.
Alisema Mwaka 2020 ni mwaka wa uchaguzi hivyo ni vyema wanawake wakajitokeza kuwania nafasi za uongozi huku akiwataka wanawake kuacha tabia ya kubezana pale mwenzao anapojitokeza kugombea nafasi za uongozi.
“Huu ni mwaka wa uchaguzi,Wanawake tujitokeze katika majimbo,tujitokeze kwa wingi katika nafasi za udiwani na kisha tujaze kwa wingi fomu za viti maalumu. Tuhamasishe wanawake wajitokeze kugombea nafasi za uongozi”,alisema.
“Wanawake ni Jeshi kubwa katika kuleta usawa lakini cha kushangaza Mwanamke ndiyo wa kwanza kumponda mwenzie. Haya tuyaache,Ukiona mwanamke mwenzio kachukua fomu ya kugombea msaidie siyo kumponda.Mimi mwenyewe nimefikia hatua hii baada ya kushikwa mkono”,aliongeza.
Aliwaasa wanawake kushikamana kuiomba jamii kwa kuwashika mkono wanawake wenye sifa za kuwa viongozi ili kuhakikisha idadi ya wanawake katika meza za maamuzi inaongezeka hatimaye kufikia usawa wa kijinsia.
Alisema kuhusu suala la ushiriki wa wanawake katika meza ya maamuzi serikali imechukua hatua kadhaa ili kuondoa vizingiti vinavyowazuia wanawake wasishiriki kikamilifu katika meza ya maamuzi.
“Changamoto iliyopo ni uchache wa wanawake wenye uwezo wa kugombea nafasi mbalimbali iwe kwenye uongozi wa kisiasa,biashara,asasi za kiraia na sekta binafsi. Ni jukumu letu kama watetezi wa haki za wanawake kushawishi wanawake wenye uwezo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika Nyanja tofauti”,alisema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika lisilo la kiserikali la Women Fund Tanzania (WFT) Prof. Ruth Meena Prof. Meena kutoka WFT,alisema licha ya wanawake kuwa nguzo kuu ya Maendeleo katika kukuza uchumi wa nchi bado wanabeba mzigo mkubwa wa kulea na kuendeleza kizazi cha taifa bila nyenzo wezeshi katika kaya na jamii zao hali inayosababisha umaskini na ufukara wa dunia kuendelea kubeba sura ya mwanamke na msichana.
Prof. Meena kutoka WFT inayofanya shughuli za utetezi wa haki za wanawake na ujenzi wa tapo ya wanawake Tanzania,alisema pamoja na ongezeko la wanawake na wasichana katika uongozi na meza za maamuzi lakini bado ushiriki wao katika katika meza hizo za maamuzi haupo sawia katika Nyanja zote za kisiasa,kiuchumi na hata kiustawi wa jamii.
“Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanyika kuleta mabadiliko kwenye sera na sheria za nchi,bado kuna mifumo kandamizi na ya kiubaguzi katika mifumo hi, hivyo kuna umuhimu wa uwajibikaji zaidi kwenye kubomoa mifumo kandamizi hususani mfume dume”,alisema.
Kongamano la Kuadhimisha na Kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 baada ya Mkutano wa Beijing likiongozwa na Kauli mbiu ya ”Uwajibikaji wa uongozi kwenye kujenga kizazi cha usawa wa jinsia” limeandaliwa na Mtandao wa Wanawake na katiba, Uchaguzi na Uongozi kwa ufadhili wa Women Fund Tanzania, Global Affairs Canada, Embassy of Ireland, High Commission of Canada na WiLDAF
No comments :
Post a Comment